Advertisements

Friday, August 29, 2014

ANGALIA PICHA DADA HUYU NA SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA

Msichana anayetambulika kwa jina moja la Mary (23) anayedai kuchoshwa na kazi ya kubebeshwa madawa ya kulevya.
Msichana aliyejitambulisha kwa jina moja la Mary (23), mkazi wa Dar ambaye ni mwenyeji wa Nyegezi, Mwanza, ameangua kilio na kusema; ‘nabebeshwa madawa ya kulevya (unga), nalipwa kiduchu hadi nimechoka’.Awali, gazeti hili lilitonywa na vyanzo vyake juu ya kuwepo kwa ishu hiyo maeneo ya Manzese, Dar ambapo uchunguzi ulifanyika na kumnasa binti huyo ambaye alifunguka kila kitu.
Akizungumza na wanahabari wetu kwa uoga mkubwa, Mary alidai kwamba alichukuliwa kutoka kijijini kwao huko Nyegezi ambapo alipofikishwa Dar, alijikuta akiunganishwa kwenye mtandao wa kuuza ‘unga’. 
“Nililetwa Dar mwaka jana na mwanaume mmoja, aliniahidi kunitafutia kazi, niliishi naye kama mtoto wake.“Zilipita kama wiki mbili tangu aliponileta bila kuniambia nitafanya kazi gani, siku moja ndipo akanipeleka Mitaa ya Magomeni (Dar) na kuniambia nitakuwa nafanya shughuli za kuuza unga huku nikiishi nyumbani kwake na yeye ndiye bosi wangu. 
“Nilishangaa sana kuona ile ndiyo kazi niliyoahidiwa kuja kuifanya Dar. Nilianza kumlilia bosi wangu anirudishe kwetu Mwanza lakini alinigomea, hata pale nilipotafuta kisingizio cha kumwambia nimemkumbuka mama yangu, aliniambia nimtumie nauli aje Dar,” alisema binti huyo akilengwalengwa na machozi.
Baadhi ya madawa ya kulevya yaliyowahi kunaswa.
Aliendelea kusimulia kwa majonzi kwamba, siku hadi siku amekuwa akiiona dunia ikimuelemea kwa kuwa amechoka na hayupo radhi kufanya shughuli hiyo, kwani mbali na hatari yake haoni manufaa anayopata. 

Alisema, awali alikuwa akilipwa Sh. 3,000 kila siku kwa kupakia kwenye paketi na alipobadilishiwa kitengo na kuanza kuhesabu kete na kubebeshwa amekuwa akilipwa kiduchu, yaani Sh. 50,000 kwa mwezi. 

“Hii kazi sitaki hata kuisikia, nimeshafanya kwa mwaka mmoja sasa, sijapata faida yoyote kwani nalipwa kiduchu huku nikiishi kwa hofu muda wote hivyo nimechoka.“Kuna kipindi mama yangu alikuja na kufikia kwake, alimnyanyasa na kumnyima nauli ya kurudi Mwanza. Alikuwa ananiambia kama vipi nikajiuze nipate nauli ya mama yangu.
Kamanda Godfrey Nzowa.
“Sikuwa tayari kufanya hivyo, mama yangu akasaidiwa na jirani akasafirishwa kurudi kijijini Mwanza,” alisema na kuongeza:
“Kuna wakati ananitishia maisha endapo nitatoa siri popote, jambo ambalo limenifanya nikose uhuru na amani ya maisha, ndiyo maana nimeshukuru kukutana na magazeti ya Global Publishers nitue huu mzigo.” 
Katika kile kinachozidi kumtia hofu ni pale alipoambiwa siku chache zijazo ataanza kusafirisha unga nchi mbalimbali na kupata utajiri mnono jambo ambalo hataki kulisikia, kwa kuwa anaogopa kuozea jela hivyo kikubwa anachohitaji ni msaada wa nauli ya kurudi kwao Mwanza akamsaidie mama yake ambaye ni mzee na ni mgonjwa. 
Kwa yeyote aliyeguswa na habari ya mwanadada huyu na anahitaji kumsaidia nauli ya kumrudisha Mwanza, awasiliane nasi kwa namba 0719595558.

1 comment:

Anonymous said...

This is crime.How comes to serve this lady? Akamatwe yeye na huyo nyangumi wake. Tatizo hakuna serikali thabiti tanzania