Advertisements

Tuesday, November 24, 2015

Lowassa awapiga chenga ya mwili polisi

MTZ DAILY.indd
Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, imedaiwa kuwa amewashitukiza polisi wa mkoa wa Shinyanga, baada ya kwenda mjini Kahama bila kupata msafara wa polisi.

Lowassa aliondoka alikwenda Kahama kuwajulia hali wachimbaji watatu waliolazwa katika hospitali ya wilaya, baada ya kuokolewa, kufuatia kufunikwa na kifusi mgodini na kukaa humo kwa siku 41.

Lowassa licha ya kuwa chama cha upinzani, lakini anahitaji kupata ‘escot’ ya polisi kutokana na kuwahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mtoa habari aliyekuwa katika msafara wa Lowassa kuelekea wilayani Kahama kuwapa pole wachimbaji hao wa ajali ya machimbo ya Nyangarata, alisema polisi walikuwa hawajaweka ulinzi wa kumsindikiza Lowassa wakati wa kutoka Mwanza kwenda Kahama na kurudi.

Hata hivyo, alisema wakati wakirejea kutoka Kahama, njiani walikutana na gari moja la polisi ambalo lilionekana ‘kuwafukizia’, lakini lilipotezwa kwa spidi ya magari yaliyokuwa yakitumiwa katika msafara wa Lowassa.

Akizungumzia uwepo wa Lowassa katika mkoa wake, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema ziara aliyoifanya waziri mkuu huyo mstaafu, ilikuwa binafsi ingawa alipata taarifa ya ujio wake.

“Hiyo ni ziara yake binafsi, lakini taarifa za ujio wake katika mkoa wangu nilizipata,” alisema Kamugisha.

Hata hivyo, pamoja na Kamanda Kamugisha kusema kuwa Polisi ilikuwa na taarifa za kuwapo kwa Lowassa mkoani humo, habari zaidi zinaeleza kuwa taarifa ambazo polisi walikuwa nazo ni kuwa mwanasiasa huyo angekwenda Shinyanga leo, badala ya jana.

AWAFARIJI, AWAJAZA MAPESA WAATHIRIKA
Katika ziara hiyo, Lowassa aliwapa pole wachimbaji walionusurika kufa, baada ya kufukiwa na kifusi katika machimbo ya Nyangarata, Kahama, mkoani Shinyanga.

Wachimbaji hao hivi sasa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya wilaya ya Kahama.

Akitoa pole hizo, Lowassa aliwataka waathirika hao kumshukuru Mungu kutokana na kuwanusuru katika janga hilo ambalo hakuna mtu aliyetegemea kutokea na wao kupona, baada ya ndugu, jamaa na marafiki na jamii kukata tamaa ya kupatikana wakiwa hai.

Sambamba na pole hizo, Lowassa aliwakabidhi msaada wa Sh. 2,000,000 wa waathirika hao wanne huku kila mmoja akipatiwa Sh. 500,000 na kuwataka wawe na subira katika kipindi chote cha matibabu wanayoendelea kupatiwa.

Waathirika waliopata msaada huo wa Lowassa ni Chacha Wambura, Amos Mhangwa, Msafiri Gerard na Joseph Bulule.

Onyiwa Moris aliyeokolewa baada ya kukaa mgodini na wenzake kwa siku 41, akifariki dunia juzi hospitalini hapo, baada ya hali yake kubadilika ghafla kutokana na kupata matatizo ya kushindwa kupumua.

Walifunikwa na kifusi hicho Oktoba 5, mwaka huu, katika mgodi huo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, baada ya kutembelewa na Lowassa, Bulule alisema wanafarijika na ujio huo na kuona hawako peka yao, licha ya juzi kumpoteza mwenzao (Onyiwa).

Naye Dk. Fredrick Malunde akizungumza kwa niaba ya jopo la madaktari wanaowashughulikia waathirika hao, alisema hali za wagonjwa hao hivi sasa zinaendelea kuimarika tofauti na awali huku huduma zaidi zikitolewa kuhakikisha wanaimarika kiafya.

Wachimbaji hao wamekuwa wakitembelewa na watu mbalimbali hospitalini hapo kwa lengo la kuwapa pole na msaada wa hali na mali.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Mzee Lowasa, Jee? umekwishastaafu na ufugaji wa ng'ombe? Mzee unazungukazunguka kama kwamba uchaguzi haujafanyika bado? Pumzika mzee kwani afya yako ni dhaifu, kwani hata sisi wapiga kura tumekwishaanza maisha mapya na tunajaribu kukusahau.