Advertisements

Saturday, July 23, 2016

KOFFI ATIMULIWA NCHINI KENYA

TAZAMA MAHOJIANO YA KOFFI NA THE CITIZEN
Nairobi, Kenya
SAA chache baada ya kusambaa mitandaoni kwa video inayomuonesha gwiji wa muziki wa dansi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Koffi Olomide akimpiga mateke mmoja kati ya madansa wake wa kike, msanii huyo ameibuka na kukanusha madai hayo na kueleza kwamba alikuwa akiwalinda madansa wake wasiibiwe lakini hiyo haijazuia serikali ya nchi hiyo kumtimua.

Katika tukio hilo lililotokea muda mfupi baada ya Koffi kutua uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi akiwa na madansa wake, nguli huyo anaonekana akimvurumishia mateke dansa huyo huku maafisa wa polisi waliokuwa uwanjani hapo wakimtuliza.

“Mimi ni mtu ninayewaheshimu wanawake, siwezi kufanya tukio kama hilo. Kilichotokea ni kwamba nilikuwa nikifanya mahojiano na waandishi wa habari, nikasikia kelele nyuma yangu. Kugeuka nikamuona mtu mmoja ambaye baadaye niliambiwa ni kibaka wa mifukoni, akitaka kuwaibia madansa wangu, ikabidi nimrushie teke ili kumzuia asiwaibie,” alisema Koffi katika mahojiano maalum na Kituo cha Runinga cha Citizen.

“Narudia tena, sikumpiga dansa wangu wala sikuwa na sababu ya kufanya hivyo, hao wanaoieneza video hiyo wanataka watu wasije kwenye shoo yangu, nawaomba mashabiki zangu na wanawake wote wasiamini kinachozungumzwa,” alisisitiza Koffi.

Ili kuonesha kwamba yeye na dansa wake huyo hawana tatizo, muda mfupi baada ya kutokea tukio hilo, Koffi na dansa huyo walijirekodi video na kuirusha mtandaoni na hata kwenye mahojiani hayo, baada ya kumaliza kukanusha taarifa hizo, Koffi alijumuika na madansa wake kuimba kipande cha wimbo wake maarufu wa Selfie (Ekotite).

Kufuatia tukio hilo, Koffi alikamatwa na polisi na kuhojiwa kabla ya baadaye kurudishwa kwao kwa ndege ya Shirika la Kenya Airways chini ya ulinzi mkali, hivyo kufutwa kwa shoo kubwa iliyokuwa ifanyike leo Boma, Nairobi usiku wa leo.

CHANZO:GPL

No comments: